Wizara ya Fedha

Wizara ya Fedha

Share

Ukurasa Rasmi wa Wizara ya Fedha Tanzania.

Photos from Wizara ya Fedha's post 14/06/2026

Serikali imesema kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika ndani ya mwezi Septemba mwaka huu, hatua inayotarajiwa kuimarisha usafiri wa anga na kulipa hadhi zaidi jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya nchi.

Akizungumza wakati alipotembelea na kuona maendeleo ya mradi huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), alisema ujenzi wa uwanja huo umefikia hatua za mwisho ambapo miundombinu mikubwa ikiwemo njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na maeneo ya maegesho ya ndege imekamilika kwa kiwango kikubwa.

Mhe. Balozi Omar, alisema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Afrika Growing Together Fund (AGTF), ukiwa na lengo la kujenga uwanja wa kisasa utakaoendana na mahitaji ya Mji Mkuu wa nchi.

“Dodoma ni makao makuu ya nchi, hivyo ilikuwa muhimu kuwa na uwanja wa ndege wa kisasa unaoweza kukidhi ongezeko la shughuli za kiuchumi, kiserikali na kijamii,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa, Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyotolewa na watalaamu, sehemu ya kwanza inayohusisha miundombinu ya uwanja imefikia asilimia 86.73 ya utekelezaji, huku sehemu ya pili inayohusisha majengo muhimu ikiwemo jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege na jengo la zimamoto ikiwa imefikia asilimia 75.1.

“Uwanja huu utakuwa miongoni mwa viwanja vikubwa nchini, ukiwa na njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60, pamoja na maegesho makubwa ya ndege yatakayowezesha kuhudumia ndege nyingi kwa wakati mmoja” aliongeza Mhe. Balozi Omar.

Aidha Mhe. Balozi Omar, alisema Kukamilika kwa Uwanja huo kunatarajiwa kuufungua zaidi mji wa Dodoma kwa safari za ndani na kimataifa, huku ukiongeza mvuto wa uwekezaji, kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kuwa jengo la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka, jambo linalotarajiwa kuongeza uwezo wa Dodoma kupokea wageni wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, jengo la zimamoto la kiwango cha kimataifa, majengo ya kuzalisha umeme na jengo la hali ya hewa lenye vifaa vya kisasa vya usimamizi wa usafiri wa anga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya (Mb) alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati na ya kielelezo inayotekelezwa nchini chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema mradi huo umebuniwa kwa mtazamo wa muda mrefu, ukiwa na uwezo wa kupanuliwa hatua kwa hatua kulingana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga nchini.

“Uwanja huu umejengwa kwa viwango vya kisasa vya kimataifa na unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vya ndege vya kisasa zaidi nchini mara utakapoanza kutumika” alisema Mhe. Kasekenya

Alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili ahadi ya kuanza kwa shughuli za uwanja huo mwezi Septemba itimie, huku akibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri na kukuza uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji mkubwa wa kimkakati.

Katika Ziara hiyo Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis M***a Omar, aliambatana na Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Mhe. Laurent Luswetula, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour pamoja na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi wakiwemo Wakala wa Barabara nchini (Tanroads).

14/06/2026

TANGAZO

Photos from Wizara ya Fedha's post 13/06/2026

Serikali imezitaka taasisi zote za umma nchini kuimarisha usimamizi wa mali za Serikali kwa kuhakikisha taarifa zote za mali zinaingizwa na kutunzwa katika Mfumo wa Serikali wa Usimamizi wa Mali (GAMIS), ili kuongeza uwajibikaji, kuimarisha matumizi ya rasilimali za umma na kupunguza hoja za ukaguzi.

Maagizo hayo yametolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Mnyema, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Maafisa Masuuli wa Taasisi za Umma kutoka Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Idara zinazojitegemea na taasisi nyingine zinazofunga hesabu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro, yaliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Uuguzi na Ukunga mkoani Pwani .

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Bi. Mnyema alisema mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wakuu wa taasisi za umma katika kusimamia mali za Serikali kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma Sura ya 348, Kanuni za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 pamoja na miongozo mbalimbali inayosimamia eneo hilo.

“Mali za umma ni rasilimali muhimu zinazowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo, huku wastani wa asilimia 70 ya bajeti za taasisi za umma ukitumika katika ununuzi unaozalisha mali hizo, usimamizi wake unapaswa kuzingatia uwajibikaji, ufanisi na utii wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa”,alisema Bi. Mnyema.

Aidha, taasisi hizo zimetakiwa kuhakikisha mali chakavu, sinzia, ziada na zilizokwisha muda wa matumizi zinaondoshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo kabla ya Septemba 30, 2026 ili kuimarisha ufanisi wa matumizi ya mali za umma.

Katika hatua nyingine Bi. Mnyema, amezitaka taasisi za umma kuwasilisha taarifa za ajali, hasara na upotevu wa mali kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali ndani ya siku 30 tangu tukio litokee na mali zilizopata ajali au uharibifu zifanyiwe matengenezo mara baada ya kupata kibali husika.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mali za Serikali Bw. Ismael Ogaga, alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamizi wa mali za Serikali.

Alifafanua kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata uelewa wa kina kuhusu sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa mali za umma, jambo litakalosaidia kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za Serikali na kupunguza hoja za ukaguzi.

Aidha, alisema Wizara ya Fedha itaendelea kutoa mafunzo hayo katika mikoa yote nchini ili kuhakikisha watumishi wa umma wanapata maarifa na stadi zinazohitajika katika kusimamia mali za Serikali.

Kwa upande wao mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dkt. Revocatus Mushumbusi, alisema kuwa watahakikisha wanayafanyia kazi yote waliyojifunza ili kuimarisha usimamizi wa mali za umma katika taasisi zao.

Aidha, aliiomba Wizara ya Fedha kuendelea kutoa mafunzo k**a hayo kwa watumishi wa ngazi za chini wanaoshiriki moja kwa moja katika shughuli za usimamizi wa mali, ili kuongeza uelewa na kuhakikisha utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu unafanyika kwa ufanisi katika ngazi zote.

Katika mafunzo hayo jumla ya mada sita ziliwasilishwa ikiwemo majukumu ya Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali na Upungufu wa Taasisi za Umma kwenye usimamizi wa mali, usimamizi wa vifaa vya kuhifadhia fedha, mali za thamani na nyaraka muhimu, usimamizi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali (GAMIS), usimamizi wa ajali na potevu za mali za umma na mwongozo wa kushughulikia madai ya fidia pamoja.

Hadi sasa Wizara ya Fedha imeshafanya mafunzo hayo kwa Maafisa Masuuli katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Pwani.

Photos from Wizara ya Fedha's post 13/06/2026

Wizara ya Fedha imewakutanisha wadau wa ununuzi na ugavi kutoka katika taasisi za umma nchini, katika kikao kazi cha uthibitisho wa Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu (2026 – 2037).

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kimelenga kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau hao, yanayolenga kuboresha na kuimarisha Mkakati huo kabla ya kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa.

Akizungumza wakati akifunga kikao kazi hicho mkoani Morogoro, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Mhina, alisema lengo la kikao hicho ni kupata maoni ya wadau ili kuboresha rasimu ya mkakati ili kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa ugavi, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma pamoja na kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu.

‘‘Tumepokea maoni yote mliyoyatoa na sisi k**a Wizara jukumu letu ni kwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha maeneo yote tuliyoafikiana na kisha tutarejesha kwenu tena ili muweza kuhakiki k**a yale yote tuliyokubaliana yamefanyiwa kazi’’, alisema Bw. Omari.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu utasaidia taasisi nunuzi nchini kuendesha shughuli za mnyororo wa ugavi kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia malengo ya DIRA 2050, matakwa ya Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.

Wakizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi wa Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro na Rufiji, Bw. Arnold Mapinduzi, alisema kuwa ushiriki wa taasisi mbalimbali katika kupitia rasimu hiyo ni muhimu katika kuhakikisha masuala ya uhifadhi wa mazingira yanajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya ununuzi na ugavi nchini.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Bi. Upeo Sanga, amesema kikao hicho kimewapa wadau fursa ya kujadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu wa mwaka 2026–2037 kabla ya kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa.

Kikao hicho kilichowakutanisha washiriki kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Chuo Kikuu Mzumbe, pamoja na wadau wengine muhimu katika mnyororo wa ugavi, kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dar to Moro, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia tarehe 11 hadi 12 Juni, 2026.

Photos from Wizara ya Fedha's post 13/06/2026

Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Sehemu ya Ajali na Fidia katika Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Dkt. Wenceslaus Sobayi, amewataka Maafisa Masuuli na viongozi wa taasisi za umma nchini kuimarisha usimamizi wa mali za Serikali kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za umma na kupunguza hoja za ukaguzi.

Akifungua mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Wakuu wa Taasisi za Umma yaliyofanyika katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Mkoa wa Katavi, Dkt. Sobayi alisema Serikali imeamua kuendelea kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wakuu kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika usimamizi wa mali za umma.

Alibainisha kuwa uhakiki uliofanywa na Wizara ya Fedha katika taasisi mbalimbali za umma kwa miaka ya fedha 2023/24 hadi 2025/26 umeonyesha mapungufu kadhaa, ikiwemo kutokuwepo kwa nyaraka muhimu za umiliki wa mali, kutoingizwa kwa taarifa za mali kwenye Mfumo wa Serikali wa Usimamizi wa Mali (GAMIS), kutowiana kwa taarifa za mali pamoja na uwepo wa mali chakavu, sinzia na ziada.

“Upungufu huu unaifanya Serikali kuendelea kubeba gharama kubwa za ununuzi na matengenezo ya mali huku ukiendelea kuchochea hoja za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),” alisema Dkt. Sobayi.

Dkt. Sobayi alisisitiza kuwa Maafisa Masuuli wana wajibu wa kuhakikisha mali zote za umma zinaingizwa kwenye mfumo wa GAMIS, zinatunzwa ipasavyo, zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa na taarifa za ajali, upotevu au hasara za mali zinawasilishwa kwa wakati kwa mamlaka husika.

Aidha, aliwataka washiriki kutumia mafunzo hayo k**a fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zitakazosaidia kuimarisha uwajibikaji na kuongeza thamani ya uwekezaji wa Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe Bi. Shamim Daudi Mwariko, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa mafunzo hayo yenye manufaa makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha aliiomba Wizara kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara, hususan yanayohusu matumizi ya Mfumo wa GAMIS, Ili kuongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha uwajibikaji na kuakikisha usimamizi bora wa mali za umma.

Nae Msimamizi wa Mali za Serikali Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. George Kanyama alieleza kuwa Wizara imeendelea kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mali za umma kwa kufanya marekebisho katika Sheria ya Fedha za Umma Sura ya 348 na kutunga Kanuni za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024. Hatua hizo zinalenga kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za Serikali.

Vilevile, aliwakumbusha Maafisa Masuuli umuhimu wa kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi na kuonyesha uongozi wa mfano katika kulinda mali za umma. Alisisitiza kuwa mali hizo ni rasilimali za wananchi wote ambazo zimewekwa chini ya usimamizi wao kwa niaba ya Taifa, hivyo zinapaswa kutunzwa na kusimamiwa kwa umakini mkubwa.

Mafunzo hayo yanawakutanisha Wakuu wa Taasisi za Umma kutoka mikoa ya Katavi na Rukwa, yakilenga kuimarisha usimamizi wa mali za umma kuelekea mwaka wa fedha 2026/27.

Photos from Wizara ya Fedha's post 13/06/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered anayemaliza muda wake, Bw. Herman Kasekende, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa benki hiyo, Bw. Geoffrey Mchangila, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Omar alimshukuru Bw. Kasekende kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya benki nchini na kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, alimpongeza Bw. Mchangila kwa kuteuliwa kuongoza benki hiyo, akiahidi ushirikiano wa Serikali katika kuendeleza ukuaji wa sekta ya fedha na benki, kwa manufaa ya uchumi wa Taifa na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.

Photos from Wizara ya Fedha's post 12/06/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameshiriki kwenye Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Leo tarehe 12 Juni, 2026, ambapo Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni rasmi, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu huku ikiheshimu uhuru wake wa kisheria na kitaasisi, ili kuhakikisha taasisi hiyo inatekeleza kikamilifu majukumu yake katika kusimamia uthabiti wa uchumi wa nchi.

Alisema ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Benki Kuu, hususan katika masuala ya sera za fedha na sera za kibajeti, umechangia kuimarisha uchumi wa Taifa na utaendelea kuimarishwa katika kutekeleza majukumu mapya yanayoendana na mahitaji ya maendeleo ya Tanzania.

Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa, ili Taifa lifanikiwe kufikia matarajio yake ya ukuaji wa uchumi na mageuzi ya kiuchumi, ni lazima taasisi muhimu za kiuchumi, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ziendane na mwelekeo mpya wa maendeleo kwa kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na changamoto na kutumia fursa zinazojitokeza katika mazingira ya uchumi wa kisasa.

Photos from Wizara ya Fedha's post 11/06/2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akiongoza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwapongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb) na Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na Mhe. Laurent Luswetula (Mb), mara baada ya kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2026/2027, ambapo Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.33, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Photos from Wizara ya Fedha's post 11/06/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amewasilisha Mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2026/2027, ambapo amesema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.33, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26.

Mhe. Balozi Omar amesema kuwa, mapato yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 46.79 ambapo mapato ya kodi ni shilingi trilioni 36.99, mapato mengine ni shilingi trilioni 9.24 (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.977) na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi bilioni 563.1.

Aidha aliongeza kuwa Ili kuendana na dhamira ya kujitegemea katika uendeshaji wa Serikali na maendeleo, takribani robo tatu ya bajeti yote ya mwaka 2026/27, sawa na asilimia 74.2 inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani.

“Matumizi na uwekezaji katika mali zisizo za kifedha yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 54.50 pasipo kujumuisha malipo ya mtaji wa deni la Serikali. Kati ya kiasi hicho, stahiki za watumishi ikijumuisha michango ya pensheni ni shilingi trilioni 10.13, gharama za bidhaa na huduma shilingi trilioni 5.22, malipo ya riba ni shilingi trilioni 6.86, ruzuku shilingi trilioni 25.32, mafao na misaada ya kijamii shilingi trilioni 1.01, uwekezaji katika mali zisizo za kifedha shilingi trilioni 2.33 na gharama nyingine shilingi trilioni 3.63.” alisema Mhe. Balozi Omar

Aliongeza kuwa kulingana na makadirio ya mapato na matumizi hayo, kunajitokeza nakisi kwenye bajeti ya shilingi trilioni 7.71 na Serikali itaendelea kugharamia nakisi ya bajeti kwa kutumia mikopo kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa kuzingatia Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni la Serikali (2025/26 – 2027/28).

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, Katika mwaka 2026/27, Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni 15.54 ambapo Kati ya kiasi hicho, mikopo ya ndani ni shilingi trilioni 6.56, mikopo ya nje yenye masharti nafuu shilingi trilioni 6.55 na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 2.43. Aidha, Serikali inakadiria kulipa malipo ya mtaji kwa mikopo iliyoiva shilingi trilioni 7.84.

Photos from Wizara ya Fedha's post 11/06/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), alivyowasili Bungeni Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2026/2027, Leo Tarehe 11 Juni 2026.

Want your business to be the top-listed Government Service in Dodoma?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Address

Magufuli City, Treasury Street, Mtumba
Dodoma
40468

Opening Hours

Monday 09:00 - 16:30
Tuesday 09:00 - 16:30
Wednesday 09:00 - 16:30
Thursday 09:00 - 16:30
Friday 09:00 - 16:30