23/06/2026
KIDUME KILIVYOMPIGA SHERE SIMBA
Jacob Lekumbere,Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hatosahau siku alipotumia mbinu za kimedani kumkwepa simba aliyetazamana naye uso kwa uso.
Jacob akiwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro,hifadhi iliyojaa kila aina ya wanyama siku hiyo aliamka asubuhi kuelekea kwenye majukumu yake.
Akiwa porini alikutana na pundamilia,alipowaangalia wale pundamilia walikuwa wamekaa mkao wa tahadhari,Jacob machale naye yakamcheza akaanza kutembea kwa tahadhari.
Mara paaa,kutupa jicho umbali wa mita tatu simba jike yupo mbele yake,alichofanya Jacob ni kumuangalia usoni simba yule,wote wawili wakawa wanaangaliana.
Jacob alimuangalia simba na simba naye alimuangalia Jacob,Jacob alipomuona simba hachezeshi masikio wala mkia akajua simba hajakasirika.
Kilichofuata Jacob akawa kila baada ya sekunde kadhaa anarudi nyuma kidogo kidogo mpaka akafika umbali wa mita 40 huku simba akiwa amesimama anatafakari la kufanya,hatimaye Jacob akajiokoa.
Karibu Ngorongoro uone maajabu.
20/06/2026
HAKUNA MASIKA YASIYOKUWA NA KIANGAZI
Usemi usemao hakuna marefu yasiyokuwa na ncha umetimia leo ambapo jumla ya maafisa na Askari 29 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya kimuundo leo tarehe 20 Juni, 2026 katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kilichopo Mlele mkoani Katavi.
Akifunga mafunzo hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka wahitimu kuzingatia taratibu na sheria na amri zote za Jeshi la Uhifadhi
“Mmepata mafunzo ya kubadilika kimuundo kutoka raia kuwa Jeshi, matumaini yangu ni kuwa kila mmoja wetu hapa mtabadilika na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kusimamia uhifadhi na rasilimali za nchi”,alisema Meja Jenerali (Mst) Semfuko.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Mhe. Majid Mwanga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kuwa mfano mwema wa uzalendo, maadili na ujasiri katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amewahimiza wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuimarisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange amesema ushirikiano uliooneshwa kati ya TAWA na Ngorongoro katika kusimamia mafunzo hayo unaonesha kuimarika kwa Jeshi la Uhifadhi nchini na ari ya kusimamia rasilimali za Wanyamapori na Misitu.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo mkuu wa mafunzo Meja Breyman Rulenguka amesema Jumla wa watumishi 29 wamefaulu na kupata alama za kuridhisha ambapo mwanafunzi mmoja pekee hakuweza kuhitimu kutokana na sababu za kiafya.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa katika kituo hicho kwa lengo la kuimarisha Jeshi la Uhifadhi na utendaji kazi wake.
16/06/2026
DUME LA RIKA UMASAINI NDIO SAFARI YA KUAGA UJANA.
Katika jamii ya Kimaasai, maisha ya mwanaume hupitia hatua mbalimbali za kimila zinazoonyesha ukuaji, Miongoni mwa hatua hizo muhimu ni kufanyiwa sherehe inayojulikana kwa jina la Orkiteng le Sirit ikimaanisha ni mwisho wa ujana na kuingia uzeeni.
Katika hatua hii ambapo mtu anatawazwa kuingia rika la uzee, wazee wa jamii hiyo huchagua Dume la rika ambalo lina afya njema na lililohasiwa tangu utoto wake, dume hili siku ya shughuli ndio hutolewa mwanzo kwenye boma lenye Ng’ombe wengi na kumwagiwa maziwa kisha hunyongwa hadi kufa.
Sherehe ya Orkiteng le Sirit, si sherehe ya kawaida bali ni tukio la heshima kubwa linalofanyika kwa kufuata mila na desturi za kale zilizorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kwa jamii ya Kimaasai, ni hatua ya ukamilifu wa mwanaume na uthibitisho kwamba ametimiza majukumu yake ya kifamilia na kijamii, kufanyiwa sherehe hii hakuangalii umri ila inazingatia jinsia kwa kuwa anayefanyiwa sherehe hii ni mwanaume pekee, vigezo vinavyoangaliwa ili mwanaume afanyiwe sherehe hii, ni lazima awe ameoa, awe na watoto wa k**e na kiume na awe mtu mwema na maadili katika jamii.
Akizungumza wakati wa sherehe hiyo, Alaigwanani wa kabila la kimasai Maningo Rinjo amesema viongozi wa mila wa ukoo k**a (Laizer, Mollel, Laitayo, Ngidong’i) ndio wenye jukumu la kumchagua dume atakayechinjwa baada ya kujiridhisha kuwa ana sifa zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kimaasai ili kutekeleza jukumu hilo la kijamii ambalo linahudhuriwa na ndugu wote wa familia na jamii yote ya wamasai inayozunguka Kijiji hicho.
Alaigwanani Olonyori Lemoyan kutoka Ukoo wa Laizer Kata ya Nainokanoka Ngorongoro alisisitiza kuwa si kila mwanaume anastahili kufanya sherehe ya Orkiteng le Sirit, moja wa masharti muhimu ili mwanaume afanyiwe tukio hilo kuwa
na familia yenye watoto wa k**e na kiume, awe na mali na uelekeo wa maisha, mtu anayejali watu na awe ni rafiki wa ukoo wake na jamii inayomzunguka pamoja na kupata ridhaa ya ukoo wake kufanya sherehe hiyo.
Wakati wa sherehe hizo baada ya dume kunyongwa na kutolewa nyama zake, mwanaume anayehitimu (anayepandishwa rika) pamoja na mke wake na mama yake mzazi wanatakiwa hukalia utumbo wa dume hilo k**a ishara ya kuaga rasmi ujana na kuingia katika hatua ya uzee. Kitendo hicho hubeba maana kubwa ya kiutamaduni na kuashiria mwanzo wa jukumu jipya ndani ya jamii na kuachana na usharobaro na mambo yote ya ujana.
Baada ya taratibu hizo kukamilika, rika la Korianga huungana na mwenzao aliyeingia hatua ya uzee timilifu huimba nyimbo za furaha na heshima huku wakielekea bomani, wakimpongeza mwenzao kwa kufikia hatua hiyo adhimu. Nyimbo hizo huashiria kukubalika kwake rasmi katika kundi la wazee na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mila, desturi na maamuzi yanayohusu ustawi wa jamii.
Orkiteng le Sirit si tu sherehe ya kuchinja dume laa hasha, ni alama ya mafanikio ya maisha, uwajibikaji wa kifamilia na heshima ya kuwa mzee katika jamii ya Kimaasai. Hatua hii ni urithi wa kipekee unaoendelea kuunganisha vizazi na kuhifadhi utamaduni wenye thamani kubwa kwa jamii.
14/06/2026
UZIO UMEANGUSHWA, MWALI KATOKA NJE
Hayawi hayawi sasa yamekuwa na mwanzo wa ngoma ni lele, hatimaye Faru weupe walioingizwa nchini kutoka Afrika kusini na kuhifadhiwa kwenye uzio maalum tarehe 13 Juni, 2026 wameachiwa huru kujivinjari katika viunga vya kreta ya Ngorongoro ili kuungana na wenyeji wao Faru Weusi katika Kasoko ya Ngorongoro.
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande ameongoza timu ya wizara,menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wa AndBeyond kuwaachia faru hao ambao idadi yao ni 17.
Faru hao wameletwa nchini na kupandikizwa Kreta ya Ngorongoro mahsusi kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, utafiti na elimu kutokana na nchi ya Tanzania kuonekana kuwa ni sehemu salama kiulinzi, Kiuhifadhi na mazingira mujaarabu kwa spishi ya Faru hao ambao wapo kwenye kundi la Wanyama waliopo hatarini kutoweka.
Mhe. Chande ameipongeza kampuni ya AndBeyond kutokanana na kutambua umuhimu mkubwa wa Uhifadhi na utafiti katika nchi mbalimbali duniani huku akipongeza uongozi na Askari wa Ngorongoro kwa kuwa mstari wa mbele kuwalea, kuwatunza, kuwahifadhi na kulinda Faru Weupe ambao walitoweka katika Nchi yetu kwa takribani miaka 300 iliyopita.
Akizungumza katika hafla hiyo mkurugenzi wa wanyamapori wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Alexander Lobora amesema mchakato wa kuwaleta wanyama hao nchini utatoa fursa kwa Wadau wa utafiti na mafunzo kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Abdul-Razaq Badru amesema Ngorongoro ni sehemu salama kwa uhifadhi,utafiti na mafunzo ambapo ametoa wito kwa wadau kuendelea kuitumia mamlaka hiyo katika shughuli hizo.
Faru hao weupe 17 kuachiwa huru na kutamba ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ni Mwanzo wa Safari ya awamu ya pili kuleta Faru Weupe 18 kutoka Afrika Kusini kwa siku zijazo.
14/06/2026
KUMBE KAMISHNA BADRU YUPO FITI KINOMA
Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameongoza mbio za Fame Marathon zilizofanyika leo tarehe 14 Juni, 2026 katika mji wa Karatu mkoani Arusha.
Mbio hizo zilizokuwa na umbali wa Kilomita 21, 10, 05 na 02 zimeratibiwa na Hospitali ya Fame iliyopo Karatu na kuhusisha takribani wakimbiaji 650 kutoka ndani na nje ya Nchi.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mbio hizo Kamishna Badru ameeleza kuwa Uhifadhi endelevu ni pamoja na kushirikiana na Jamii zinazozunguka hifadhi katika programu ambazo zina manufaa kwa Jamii na kutoa tabasamu kwa wagonjwa mbalimbali wanaopata huduma kwenye Hospitali na Fame na nyinginezo
Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Hospitali ya FAME Bw. William Mhapa ameleeleza kuwa mbio hizo zinafanyika kwa mara ya tatu kwa lengo kushirikiana na jamii kuchangia mahitaji mbalimbali ya wagonjwa wanaofikishwa hospitali ya FAME kupata huduma za dharura na kutoa msaada kwa jamii za Karatu, Ngorongoro na maeneo jirani