14/06/2026
KATIBU WA NEC AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO, ASIKILIZA CHANGAMOTO ZA WANANCHI LINDI
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Abdalla Hamid, ameanza ziara yake mkoani Lindi kwa kusikiliza maoni na changamoto za wananchi pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Lindi.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ukumbi wa Dockyard Hall, Leo tarehe 14 June 2026, Ndugu Rabia amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi kwa kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutafuta njia za kuzitatua ili kuboresha ustawi wa jamii.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa katika mchakato wa maendeleo.
Sambamba na hilo, ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo amepata fursa ya kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake na mchango wake katika kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Lindi.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Ndg. Juma Mnwele kwa ufafanuzi na majibu ya kina aliyoyatoa kuhusu hoja na changamoto zilizowasilishwa na wananchi, jambo lililosaidia kuongeza uelewa na kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi wao.
13/06/2026
MEYA NA MKURUGENZI LINDI WAKAGUA ENEO LA SHULE MOKA
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mbe. Twahili Mpuluji pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg. Juma Mnwele wamefanya ukaguzi wa eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari katika Kijiji cha Moka, ikiwa ni hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu katika eneo hilo.
Ziara hiyo imelenga kujiridhisha na maandalizi ya awali ya mradi huo muhimu unaotarajiwa kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wa kijiji cha Moka na maeneo jirani, pamoja na kupunguza changamoto ya umbali mrefu wanaotembea wanafunzi kufuata elimu ya sekondari.
Aidha, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, huku wakitoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali katika kulinda na kusimamia miradi ya maendeleo.
Juma Mnwele
11/06/2026
MGANGA MKUU WA MKOA WA LINDI ATEMBELEA MANISPAA YA LINDI KUJIONEA HUDUMA ZA AFYA
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Victoria Ludovick leo tarehe 11 June 2026 ametembelea Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwa lengo la kujitambulisha rasmi na kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za huduma za afya zinazotolewa katika halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo, Bi. Victoria ametembelea Kituo cha Afya Mji, Hospitali ya Wilaya ya Lindi pamoja na Kituo cha Afya Rutamba ambapo alipata fursa ya kukagua utoaji wa huduma, miundombinu ya afya na kuzungumza na watumishi wa afya kuhusu changamoto na mafanikio ya sekta hiyo.
Aidha, amewataka watumishi wa afya kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya taaluma yao ili kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Bw. Juma Mnwele, ameeleza kufurahishwa na ujio wa Mganga Mkuu wa Mkoa na kusema ziara hiyo imekuwa chachu muhimu ya kuboresha huduma za afya.
“Tunaishukuru sana Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa ujio huu. Tumejifunza mengi na tutazingatia maelekezo yote yaliyotolewa ili kuimarisha zaidi huduma kwa wananchi wetu,” amesema Bw. Mnwele.
Ziara hiyo pia iliwapa fursa viongozi hao kujadili kwa pamoja namna ya kuendelea kuboresha huduma za afya na kuimarisha usimamizi wa vituo vya kutolea huduma katika Manispaa ya Lindi.
Juma Mnwele
Habari na Picha BEBO 🦋
11/06/2026
MWENYEKITI WA TRAMPA NA TIMU YAKE YAKUTANA NA MKURUGENZI LINDI KUJADILI MAENDELEO YA KADA YA WATUNZA KUMBUKUMBU
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Ndg. Juma Mnwele leo tarehe 11 June 2026 ametembelewa na wageni kutoka Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) katika ofisi ya Mkurugenzi huyo, kwa lengo la kujadili masuala ya utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka pamoja na maendeleo ya kada ya watunza kumbukumbu katika halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devotha Mrope, amesisitiza umuhimu wa kutengwa kwa fungu maalumu kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Ndg. Mnwele amewataka watunza kumbukumbu kutoficha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati. Aidha, ameahidi kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi hao ili kuongeza ufanisi katika huduma za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.
Kikao hicho kimeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka serikalini kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na utunzaji sahihi wa taarifa.
Juma Mnwele
Picha na Habari BEBO 🦋
10/06/2026
LINDI YAHITIMISHA MASHINDANO YA UMITASHUMTA NA UMISSETA 2026
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2026 yamehitimishwa leo Juni 10, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi, huku wanafunzi waliofanya vizuri wakitunukiwa zawadi mbalimbali. Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Ndg. Rehema Nahale, amesema mashindano hayo yana mchango mkubwa katika kuibua vipaji, kukuza nidhamu na kuimarisha afya za wanafunzi.
Hongera kwa kushinda mashindano hayo
09/06/2026
MKURUGENZI MANISPAA YA LINDI AKAGUA MAANDALIZI YA MAONESHO YA NANENANE ENEO LA NGONGO
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Ndugu Juma Mnwele, leo Juni 9, 2026, ameongoza timu ya wataalamu wa halmashauri hiyo kutembelea eneo la Ngongo kwa lengo la kukagua maendeleo ya maandalizi ya Maonesho ya Nanenane yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mnwele amepata fursa ya kuona hatua mbalimbali za maandalizi zinazoendelea katika eneo hilo na kujionea namna wadau wanavyojipanga kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza na waandaaji na wadau waliopo eneo la maonesho, Ndg. Mnwele amewapongeza kwa kazi nzuri na juhudi wanazoendelea kuzionesha katika kuandaa maonesho hayo muhimu kwa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha, amewasisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha kila kitu kinakamilika kwa wakati.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya katika maandalizi ya Maonesho ya Nanenane nane iwapo kuna mahitaji yoyote yanayohitaji msaada wa halmashauri, yafikisheni ofisini mapema ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati na kuwezesha maandalizi kufanikiwa.” amesema Mnwele.
Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya sekta ya kilimo na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ya kiuchumi nchini.
08/06/2026
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAWANOA WAANDISHI MKOA WA LINDI
Wizara ya Katiba na Sheria imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka wilaya mbalimbali Mkoa wa Lindi kuhusu uhamasishaji wa huduma zinazotolewa kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara hiyo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Sea View Hotel, leo tarehe 8 June 2026 Manispaa ya Lindi, yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari kufikisha kwa wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na kituo hicho pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko, maoni na changamoto mbalimbali ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Erick Salila, amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kuelimisha umma kuhusu huduma za Serikali na kuwasaidia wananchi kufahamu njia sahihi za kupata huduma na kuwasilisha changamoto zao.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Ndg. Wilson Rucho, amesisitiza wananchi kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja k**a njia rasmi ya kuwasilisha malalamiko, maoni na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu huduma za Wizara.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Katiba na Sheria za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.
Je unalipi la kusema kupitia Huduma hiyo, weka Comment hapo chini
06/06/2026
DC MWANZIVA AHITIMISHA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO MANISPAA YA LINDI
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva, amehitimisha ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi iliyolenga kupitia tarafa na kata zote za manispaa hiyo kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika ziara hiyo, Mhe.Mwanziva amekagua miradi mbalimbali na kubaini kuwa mingi imefikia zaidi ya asilimia 90 ya ukamilishaji, huku baadhi ikiwa imekamilika na tayari ikitoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo, amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi iliyosalia kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Tumeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hii. Tunasisitiza miradi iliyobaki ikamilike kwa wakati ili wananchi wa Lindi waendelee kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia uwekezaji huu wa Serikali,” amesema Mhe. Mwanziva.
Amesema ukamilishaji wa miradi hiyo unaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Ziara hiyo imehusisha wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Lindi pamoja na wataalamu wa Manispaa ya Lindi, ambao wameeleza dhamira yao ya kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa ubora, ufanisi na kwa mujibu wa ratiba zilizopangwa ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
02/06/2026
DC MWANZIVA AENDELEA KUKAGUA MIRADI YA ELIMU NA AFYA KATIKA MANISPAA YA LINDI
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva, leo Tarehe 2 Mei 2026, ameongoza muendelezo wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi kwa kutembelea Shule ya Msingi Likong’o, Hospitali ya Wilaya Kikwetu, Shule ya Msingi Likotwa Rasbura, mradi wa matundu ya vyoo Rahaleo na Shule ya Msingi Mpilipili.
Ziara hiyo imelenga kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata huduma bora za elimu na afya kupitia uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhe. Mwanziva amewataka wasimamizi wa miradi na wataalamu kuhakikisha kazi zote zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.
“Miradi hii ni kwa ajili ya wananchi, hivyo lazima isimamiwe kwa uadilifu, ubora na ikamilike kwa wakati ili ilete matokeo yaliyokusudiwa,” amesema Mhe. Mwanziva.
Aidha, amesisitiza matumizi sahihi ya fedha za umma na kuwataka watendaji kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuondoa changamoto zinazoweza kuchelewesha ukamilishaji wake.
Kwa upande wao, viongozi na wataalamu wa sekta husika wamemueleza Mkuu wa Wilaya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo na kueleza kuwa wanaendelea kuchukua hatua kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa manufaa ya wananchi wa Manispaa ya Lindi.